Jumatatu, 4 Aprili 2016



Baada ya kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), kocha mkuu wa timu ya Mwadui ya Shinyanga, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ametamka kuwa lengo lake kubwa ni kuona kikosi hicho kinatwaa ubingwa wa kombe hilo na kwenda kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho.

Mwadui imefanikiwa kutinga nusu fainali baada ya kuiondosha Geita Gold inayofundishwa na kocha wa zamani wa Simba, Seleman Matola, ambapo sasa wanasubiri kuchuana na Yanga, Azam au Coastal Union au Simba.

Julio alisema kuwa sababu kubwa ya kulipigia hesabu kombe hilo la shirikisho ni kiu yake ya kuona kikosi hicho kinapata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya kimataifa.

“Sisi hatuogopi timu yoyote ile ambayo tutapangiwa kwenye mashindano haya maana malengo yetu ni kuhakikisha tunatwaa ubingwa wa kombe hili na tuna kila sababu ya kufanya hivyo kutokana na uimara wa kikosi changu ambacho kinaweza kucheza na Yanga au Azam na tukawafunga.


”Tunalitolea macho kombe hilo kutokana na kutaka kuiwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa,” alisema Julio.
source saleh jembe




Beki wa kati wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ametamka wazi kuwa hana wasiwasi na nafasi yake ndani ya Yanga kwani anaimani atarudi katika kikosi cha kwanza na kucheza kama zamani.

Cannavaro, ambaye baada ya kuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi mitatu, Alhamisi iliyopita alipata nafasi ya kucheza kwa dakika chache kwenye mchezo wa Kombe la FA, dhidi ya Ndanda na Yanga kushinda 2-1 amesema yupo tayari kwa mapambano tena.

“Tayari nimepona kabisa na nashukuru viongozi wangu wa Yanga kwa kunitafutia sehemu nzuri ya kunitibia majeraha yaliyokuwa yakinisumbua, nakishukuru pia Kituo cha Sunderland, kwani kwa muda wa wiki tatu kabla ya kujiunga na Yanga nilikuwa nafanya mazoezi pale ya kujiweka fiti.

“Nimerudi na sina wasiwasi na nafasi yangu kikosini kwani kwa nahodha yeyote duniani akirudi kutoka katika majeraha nafasi yake inakuwepo, naamini na mimi muda si mrefu nitaanza kuwa katika kikosi cha kwanza.

“Kikubwa nimefurahi nimepona muda muafaka ambao kila Mwanayanga anauhitaji mchango wangu na nasema kwamba nitawapa kile wanachokihitaji kwani nina hamu ya kucheza.

“Unajua miezi mitatu niliyokuwa nje imeniathiri kidogo, kwa sasa ninachofanya nimshawishi kocha ili aweze kunipa nafasi na niweze kucheza katika nafasi yangu niliyoiacha kwa muda mrefu,” alisema Cannavaro.


Ikumbukwe kuwa, kabla ya kuumia, alikuwa akicheza sambamba na Kelvin Yondani, lakini baada ya kuumia nafasi yake ikawa inashikiliwa na Mtogo, Vincent Bossou.
source saleh jembe


Mashabiki na viongozi wa Coastal Union wameonekana kutofurahishwa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye kutinga jezi ya Mbeya City.

Nape alivaa jezi hiyo wikiendi wakati Mbeya City ‘ilipoitumbua’ Coastal Union kwa mabao 4-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Mashabiki hao walionekana wakipinga kwenye vyombo mbalimbali vya habari na mitandaoni wakiamini haikuwa sawa.

Lakini pia walikuwa wakilalamika kuhusiana na suala hilo, wakidai kwamba wanataka kumuona pia akiwa amevaa jezi ya Coastal Union.

Hata hivyo, baadhi hasa mitandaoni nao wamekuwa wakipinga na kuamini hakuna jipya katika hilo na Nape anaweza kuvaa jezi yoyote anayotaka.

source saleh jembe

Hakuna maoni: