LUNYAMILA ALIYELIPWA SH ELFU 80 MIAKA KUMI ILIYOPITA NI BORA KULIKO WATAKAO MAMILIONI LEO...
MWAKA 1993 nilifanikiwa kumuona Abbas Gulamali
kwa mara ya kwanza uso kwa uso. Alikuwa mtaani kwetu, kwa ajili ya kufanya
mazungumzo na baba yake mdogo Edibly
Lunyamila aitwaye Emmanuel Katamba.
Lengo lilikuwa ni kumalizia mazungumzo, kumsajili
Lunyamila kutoka Shinyanga Shooting kwenda Yanga. Nikiwa na ‘masela’ wengine wa
mtaani, tulijazana dirishani na kusikiliza nusu ya sehemu ya mazungumzo, kabla
ya kushitukiwa na kutimuliwa, halafu mlinzi akakaa kulinda dirisha
tusichungulie tena.
Lakini nina uhakika hata ukimuuliza Lunyamila leo
atakuambia, Lunyamila alisajiliwa kwa kitita cha Sh milioni 1, hilo ndilo
lilikuwa dau kutoka Shinyanga Shooting kwenda Yanga!
Wakati alipojiunga Yanga, kamwe hakuna mchezaji
aliyekuwa akilipwa mshahara licha ya timu hiyo kuwa na nyota kadhaa kama Issa
Athumani na Sanifu Lazzaro ‘Tingisha’.
Mwaka 1995, Lunyamila aliondoka Yanga na kujiunga
Malindi kwa dau kubwa la Sh milioni 3.5 akiweka rekodi kwa kumzidi Nico Bambaga
ambaye alisajiliwa kwa Sh milioni 3. Wote wakaanza kula mshahara wa Sh 15,000
kwa mwezi.
Mwishoni mwa mwaka, Lunyamila na Bambaga
walirejea Yanga baada ya Malindi kuvurugika, Wazambia kama Mordon Malitoli
wakarudi kwao. Lunyamila aliiendelea kuwa nyota, shujaa na mwisho mwaka 1998
aliisaidia Yanga kufuzu kucheza Klabu Bingwa Afrika hatua ya makundi baada ya
kuifunga Coffee ya Ethiopia ambayo ilikuwa imeing’oa Al Ahly ya Misri.
Baada ya ushindi huo, Kampuni ya MIC Tanzania
maarufu kama Buzz ikajitokeza kuidhamini Yanga chini ya uongozi wa Abbas Tarimba
kama sijakosea. Ikaanza kuvaa Simu Poa, wachezaji wa Yanga wakapata neema na
kwa mara ya kwanza wakaanza kulipwa mshahara wa Sh 60,000 kwa mwezi.
Kabla walikuwa wakilipwa fedha za mapato ya geti,
timu ikishinda wanapata zaidi, sare angalau na wakifungwa wakati mwingine,
hakuna kabisa.
Siku chache zilizopita nilipoandika kuhusiana na
wachezaji wa sasa kudai fedha rundo za usajili na mshahara huku wakiwa
hawajatoa msaada wowote kwa timu zao, wako waliolaumu sana, kwamba siwatetei
wachezaji.
Kamwe sihitaji kuwa shujaa kwa kuwatetea
wachezaji, au jabali la kuwapinga, lakini naendelea kusimamia kwenye haki kwao,
pia klabu zao kwa kuwa wote ni wadau wanaoweza kuukuza mpira au kuumaliza
kabisa.
Nataka uangalie vizuri, sasa ni miaka 10 imepita
tangu Lunyamila aliporejea Yanga akiacha mshahara wa Sh 15,000 kwa mwezi kutoka
Malindi. Miaka mitatu baadaye angalau akaanza kupata mshahara wa Sh 60,000
ambao wakati mwingine walilipwa baada ya miezi mitatu.
Ramadhani Singano wa mwaka 2015, anahitaji
kulipwa Sh milioni 60 za usajili, mshahara Sh milioni 2, safi, ni mzalendo
wacha afaidike, lakini tukirejea katika kazi yake, ameifanyia nini hasa Simba?
Hajaipa hata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa au ubingwa wa Nani Mtani
Jembe unaweza kuwa mafanikio makubwa sana?
Nataka uangalie uwezo wa Lunyamila yule miaka 10
iliyopita, anzia kwa Singano, nenda kwa Simon Msuva, mchukue Mrisho Ngassa,
halafu jiulize, tunapiga hatua mbele au tunarudi nyuma.
Ubora wa Lunyamila wa miaka 10 iliyopita, bado
uko juu maradufu ya wachezaji wetu wengi nyota wa sasa. Chukua makinda na
wakongwe, kwa huruma ya kizalendo, wote tunawapigia kelele walipwe vizuri
tukiamini watafanya vizuri zaidi!
Saleh Ally anayesema ukweli anaweza kuonekana ni
chenga tu, lakini ukweli utabaki palepale kuwa kama tunakuwa na Lunyamila bora
miaka 10 iliyopita, halafu miaka 10 baadaye tunakuwa na rundo la wachezaji
wasiofikia uwezo wake, tunafikiri tunaweza kupiga hatua?
Aliyekuwa hapewi mshahara alikuwa bora, hatari,
tishio hakuna mfano. Hii pia unaweza kuiona hata ukiangalia makipa wa sasa,
mabeki wa sasa na hata viungo wa sasa, jaribu kutafuta kiungo wa Tanzania
mwenye kariba ya Issa Athumani Mgaya, Hamisi Gaga ‘Gagarino’, Method Mogella
‘Fundi’, tumia muda wako wa kutosha, halafu niambie kiungo unayemjua sasa
mwenye uwezo huo.
Kama yupo utaniambia, kama hayupo nitakuuliza kwa
nini na kuna sababu ipi sasa ya wachezaji wetu kulipwa mishahara mikubwa? Ni
fasheni tu, au timu zinataka kuonyesha uwezo wa kifedha tu?
Okwi wa leo tunayemshangaa ni sawa na Lunyamila
wa mwaka 2005 ambaye alikuwa anaelekea kumaliza soka lake.
Wachezaji wamewahi kujipima kwamba uwezo walionao
wao sasa ni mdogo kuliko ule waliokuwa nao akina Said Mwamba ‘Kizota’ enzi
zile?
AZAM FC HATUFANYI USAJILI WA KUKURUPUKA.
Licha ya klabu za Simba na Yanga kuanza kufanya usajili wa nyota
mbalimbali katika kikosi chao kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao, uongozi wa
Klabu ya Azam umetamka wazi kuwa, hauna haraka yoyote ya kufanya usajili.
Kikosi hicho cha Azam kinachonolewa na Muingereza, Stewart Hall,
mpaka sasa bado hakijaanza harakati za usajili ukilinganisha na timu za Simba
na Yanga ambazo mpaka sasa tayari zimeshasajili wachezaji zaidi ya wane kila
moja.
Msemaji wa kikosi hicho, Jaffar Idd Maganga, alisema kuwa licha za
wapinzani wao Simba na Yanga kuanza harakati za usajili, wao hawana haraka na
jambo hilo, badala yake wanajipanga ili kuweza kufanya usajili makini na kwenye
nafasi ambazo zina mapengo.
“Sisi kwa upande wetu wala hatuna shida ya kufanya usajili wa
haraka kama baadhi ya timu zilivyoanza jambo hilo, badala yake tunajipanga tu
huku tukisubiri muda ufike ndiyo tuanze kufanya hivyo.
MBEYA CITY WATAFUTA KIRAKA KIMOJA TU ?
Baada ya kufanikiwa kunasa nyota watatu, uongozi wa Klabu ya Mbeya
City, umefunguka kuwa hautafanya mabadiliko makubwa katika kikosi chake na kwa
sasa wanasaka nafasi moja pekee ya mchezaji ambaye anaweza kucheza nafasi zaidi
ya moja uwanjani.
Mbeya City imefanikiwa kumnasa beki Haruna Shamte (JKT Ruvu),
kiungo Joseph Mahundi (Coastal Union) na mshambuliaji Gideon Brown kutoka Ndanda FC huku wachezaji wake wawili,
Deus Kaseke na Peter Mwalyanzi wakitua Yanga na Simba.
Katibu wa timu hiyo, Emmanuel Kimbe, alisema kuwa kwa kiasi
kikubwa kwa sasa nafasi zote zina wachezaji na wanasaka mchezaji ambaye anamudu
nafasi zaidi ya moja.
Kimbe alisema kuwa, msimu ujao vijana watapewa nafasi katika
kikosi chao, ndiyo maana hawasajili wachezaji wengi kutokana na kuwa na vijana
wenye uwezo mkubwa.
“Tumeshawasajili wachezaji takriban watatu wa nafasi tofauti, kwa
sasa tunaangalia nafasi kama moja na tunataka mchezaji mwenye uwezo mzuri na
awe anamudu kucheza nafasi zaidi ya moja, yaani kiraka.
USISHANGAE, AMRI KIEMBA YUKO SOKONI!
Aliyekuwa kiungo wa Azam FC, Amri Kiemba, amejiweka sokoni kwa
kusema kuwa yupo tayari kutua katika timu yeyote hata kama ni Simba kutokana na
mkataba wake kuisha.
Kiemba alipelekwa Azam FC kwa mkopo wa miezi sita akitokea Simba
ambako mkataba wake umekwisha mwishoni mwa msimu uliopita, hivyo kumfanya kuwa
mchezaji huru.
Kiemba alisema kuwa kwa upande
wake yupo kikazi zaidi, hivyo iwapo timu yoyote itamtaka, atakwenda kuichezea
kwa kuwa yeye ni mchezaji huru na hata kama timu yake ya zamani ya Simba
itamfuata atakuwa tayari kurudi.
“Mimi sichagui timu ya kuichezea kwani hiyo ndiyo kazi yangu na
nipo tayari kwenda kuichezea timu yoyote ile ilimradi kukubaliana tu.
“Mipango yangu kwa sasa bado na siwezi kusema timu gani hasa inanifaa
kuichezea msimu ujao, ila yoyote ile itakayokuja hata kama ni Simba mimi nipo
kikazi zaidi.
“Kwa sasa hakuna timu hata moja iliyonifuata kutaka kunisajili kwa
kuwa walikuwa hawaelewi kama mkataba wangu umekwisha,” alisema Kiemba.KASEKE ATAKA NAMBA YA MSUVA AU NIYONZOMA!
Kiungo mshambuliaji mpya wa Yanga, Deus Kaseke, aliyetokea timu ya
Mbeya City ya jijini Mbeya, ametangaza vita kwa kiungo mwenzake, Simon Msuva au Haruna Niyonzima,
kwa kusema kuwa atajipanga kuhakikisha anapangwa katika kikosi cha kwanza.
Kaseke amesema ni lazima aonyeshe uwezo wa juu kuliko Simon Msuva
kwa kuwa anataka akiwa Yanga acheze namba 11.
Kaseke amesajiliwa na Yanga hivi karibuni ambapo amekuja kuziba
pengo la Mrisho Ngassa aliyetimkia Afrika Kusini katika timu ya Free State.
Kaseke amesema kuwa kati ya
namba tatu anazocheza 10, 11 na 7, namba 11 pekee ndiyo ambayo anaona
ataitendea haki iwapo kocha Hans Pluijm atampanga.
“Mimi nacheza nafasi tatu ambazo ni saba, 10 na 11, lakini namba
11 kwa upande wangu ndiyo ninaiona kuwa huru zaidi pindi ninapoicheza, hivyo
ningependa kocha anipange namba hiyo na nitajituma kuhakikisha napata nafasi,
najua kuna wengine wanaweza kucheza hapo lakini nikijituma najua nitapewa
kipaumbele.
“Iwapo mwalimu atanipanga katika namba hiyo, nitakuwa vizuri zaidi
kuliko hizi nyingine zilizobakia.
“Kuhusu ushindani wa namba, nimejipanga vyema hata kama kuna watu, nitajituma kadiri ya uwezo wangu kuweza kumshawishi kocha,” alisema Kaseke.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni