YANGA YALALA MECHI YA KWANZA KAGAME, OLUNGA ATESA, CANNAVARO AKOSA PENALTI
![]() |
MUUAJI WA YANGA: OLUNGA, NI HATARI... |
Yanga imepoteza kwa bao 2-1 katika mechi ya ufunguzi ya Kombe la Kagame.
Gor Mahia, mabingwa wa Kenya ndiyo walioibuka na ushindi katika mchezo huo mtamu uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 katika kipindi cha kwanza.
Lakini Gor Mahia wakazidi kutamba katika kipindi cha pili kwa kupata bao la kwanza kupitia kwa mshambuliaji wake Michael Olunga.
Olunga aliyekuwa akiisumbua ngome ya Yanga tokea kipindi cha kwanza alifunga bao hilo baada ya kuwatoka Kelvin Yondani na Mbuyu Twite.
Yanga walitangulia kupata bao katika kipindi cha kwanza baada ya Gor Mahia kujifunga baada ya krosi ya Donald Ngoma, hiyo ilikuwa dakika ya 5.
Dakika ya 16, Shakava akasawazisha kwa kichwa baada ya Juma Abdul kumuangudha Walusimbi.
Dakika ya 24, Ngoma akalambwa kadi ya pili ya njano na kutolewa nje.
Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alikuwa na nafasi ya kusawazisha kwa Yanga baada ya kupiga mkwaju wa penalty, kipa akaudaka.
Mwishoni mwa kipindi cha pili Yanga walicharuka na kushambulia mfululizo lakini haikuwazuia Gor kukomaa na kubakiza ushindi wao wa kwanza dhidi ya Yanga.
MAGULI SASA ATAKA KUWAZIDI UJANJA MAVUGO, KIIZA ILI APEWE KAZI YA KUCHEKA NA NYAVU
Mshambuliaji mwenye minguvu wa Simba, Elius Maguli, ameonekana kujiamini kupitiliza baada ya kutamka kuwa atafanya kazi yake kwa ufasaha na kuwazidi ujanja Laudit Mavugo na Khamis Kiiza ili yeye awe bora zaidi yao.
Maguli ameenda mbali zaidi kwa kusema, yeye ndiye mbadala wa straika Emmanuel Okwi aliyejiunga na Klabu ya Sonderjyske ya Denmark na siyo mchezaji mwingine yeyote.
Tayari Kiiza ameshajiunga na Simba lakini Mavugo bado yupo kwao akimalizia mechi za timu yake ya Vital’O ndipo aje nchini kujiunga na Wekundu wa Msimbazi.
Maguli alisema haangalii rekodi bali anasubiri kuona uwezo utakaoonyeshwa na wachezaji hao na atapambana nao kwa kufanya mazoezi ya nguvu kuwapiku.
“Unadhani nitaangalia eti nani kafanya nini? Siogopi lolote kwa hao jamaa ninaogombea nao namba, mimi nitapambana kwa mazoezi binafsi na tukikutana kwenye mazoezi ya wote watauona moto wangu,” alisema Maguli.
Hadi sasa Mavugo anaelezwa kufunga mabao 34 katika msimu unaomalizika huko Burundi katika michuano yote na uwezo wa kufunga wa Kiiza unafahamika tangu alipokuwa Yanga msimu uliopita.
MAGUFULI, ODINGA NDANI YA TAIFA LEO YANGA VS GOR MAHIA
Mwanasiasa maarufu wa Kenya, Raila Odinga leo anatarajiwa kushuhudia mechi ya ufunguzi ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame itakayozikutanisha Yanga na Gor Mahia ya Kenya kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Odinga ambaye ni kiongozi wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM)’ ni shabiki mkubwa wa Gor Mahia atakuwa sambamba na baadhi ya mashabiki wa timu hiyo waliosafiri kutoka Kenya kuja kuishangilia.
![]() |
ODINGA... |
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, Odinga ambaye anayedaiwa kuwa na urafiki na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, atatazama mechi hiyo kisha atakutana na baadhi ya wanasiasa na wafanyabiashara wa Tanzania.
Urafiki wa Magufuli na Odinga umethibitishwa zaidi hivi karibuni ambapo waziri huyo aliyechaguliwa kuwania urasi wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kwenda Kenya katika mazishi ya mtoto wa Odinga pia aliwahi kumuunga mkono katika kampeni za urais.
Pamoja na urafiki wake na Magufuli, Odinga ni rafiki wa karibu wa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji ambaye imeelezwa huenda akaungana nao uwanjani katika mechi hiyo.
Manji aliwahi kumualika Odinga wakati wa ufunguzi wa maduka yake makubwa ya kibishara ya Quality Centre jijini Dar es Salaam.
MWINGEREZA AFELI MAJARIBIO AZAM FC, NAFASI YAKE KUCHUKULIWA NA MKENYA
Mambo yameshaharibika kwani lile dili la kiungo Ryan Burge kutaka kuwek a rekodi ya kuwa Muingereza wa pili kucheza Ligi Kuu Bara limeshindikana na muda wowote ataondoka nchini kurudi kwao.
Kally Ongala, ndiye raia wa kwanza wa Uingereza, kucheza Ligi Kuu Bara alipozichezea Yanga na Azam, kabla ya kuachana na soka na sasa ni kocha.
Burge alisema: “Mambo yameshindikana na nitarejea nyumbani ambako nimepata timu ya kuchezea, sijajua ni kitu gani kilichokwamisha usajili wangu.”
![]() |
WANGA (MBELE) WAKATI AKIWA EL MERREIKH AKIPAMBANA NA MIGI WAKATI AKIICHEZEA APR. |
Taarifa zinaeleza baada ya ujio wa Allan Wanga, Azam FC imeona ni vizuri kumchukua Mkenya huyo na kuachana na Mwingereza huyo.
Burge alisema: “Muda wowote nitaondoka kurejea nyumbani kwa sababu kuna timu imetokea kunihitaji, siwezi kukutajia ni timu gani mpaka nitakapofika huko na kufanya nao mazungumzo.”
Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mchezo huo bila shaka ataiunga mkono Yanga ambayo ni Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni