Mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva amesema wamekikubali kipigo kutoka Azam FC lakini bado wana nafasi ya kujirekebisha.
Yanga imepokea kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Azam FC katika mechi ya mwisho ya Kundi B katika michuano ya Mapinduzi. Mechi hiyo imechezwa jana kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Msuva amesema mashabiki wasikate tamaa, waendelee kuwaunga mkono nao kupitia benchi la ufundi na wao wenyewe watajirekebisha.
"Mpira una matokeo matatu, kushinda, sare au kufungwa. Kufungwa imetutokea sisi, lakini hatuna ujanja. Nawaomba mashabiki wasikate tamaa na badala yake waendelee kutuunga mkono.
"Benchi la ufundi wameona makosa yetu, sisi wachezaji tumeona na tutayafanyia kazi na kuendelea kufanya vizuri.
"Unajua kikubwa ambacho ni kizuri tumevuka kwenda nusu fainali hivyo tuna nafasi ya kujirekebisha kwenye nusu fainali na ikiwezekana fainali," alisema.
Baada ya Yanga kupoteza kwa mabao 4-0 dhidi ya Azam FC, Simba imesema itaendelea kuchukua tahadhari kubwa kwa kila mechi yake ya Kombe la Mapinduzi.
Simba imeshinda mechi zake zote za Mapinduzi lakini haikuwa ikishinda kwa idadi kubwa ya mabao kama ilivyo kwa Yanga.
Simba inashuka dimbani Amaan mjini Zanzibar kuivaa Jang’ombe Boys katika michuano hiyo.
Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja amesema wako tayari na wanachotaka ni kufanya vizuri.
“Kila mechi ni mechi nyingine, lazima kuwa makini kwa lengo la kufanya vizuri,” alisema.
Simba inaongoza Kundi A ikiwa na pointi saba baada ya kushinda mbili na sare moja.
Iwapo itashinda leo, uhakika asilimia mia kuivaa Yanga katika nusu fainali utakuwa umepatikana.
SOURCE SALEHJEMBE